Dkt. Mwanjelwa:Fuatilieni utekelezaji wa viapo vinavyotolewa na viongozi wa umma.


Dkt. Mwanjelwa:Fuatilieni utekelezaji wa viapo vinavyotolewa na viongozi wa umma.
24
Jan
2019

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa ameiagiza Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kufuatilia utekelezaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ili kujiridhishakama viongozi wanafanyakazi kwa mujibu wa matamko pamoja na viapo vyao.

Mhe. Mwanjelwa ametoa agizo hilo hivi karibuni jijini Dodoma alipotembelea Ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa lengo la kufahamiana na kuangalia utendaji kazi wa ofisi hiyo.

Kila kiongozi wa umma anatakiwa kutoa tamko la Rasilimali na Madeni kwa Kamishna wa Maadili siku 30 baada ya kuteuliwa na kila ifikapodesemba 31 ya kila mwaka pamoja na kiapo cha Ahadi ya Uadilifu pindi anapoteuliwa kushika wadhifa serikalini.

Alisema, “lazima mfuatilie utekelezaji wa matamko na viapo vinavyotolewa na viongozi wa Umma na kuchukua hatua kali kwa viongozi wanaokwenda kinyume na matamko yao.”

Kwa mujibu wa Naibu Waziri Mwanjelwa, eneo la ufuatiliaji wa matamko na viapo kwa viongozi wa Ummma lina pengo kwasababu wapo viongozi wanaosoma matamko na kula kiapo cha Ahadi ya Uadilifu, lakini maisha yao ni tofauti na viapo walivyokula.

Katika hatua nyingine, Mhe. Mwanjelwa amewataka watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya viongozi kufanyakazi kwa uzalendo na kuwa waadilifu wa hali ya juu na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

Alisema, nyinyi chapeni kazi, twende na kasi ya mabadiliko yaliyopo leo, kuweni wavumilivu, changamoto zilizopo, lazima mkabiliane nazo.

“Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma hamtakiwi kuishi kimazoea au kufanyakazi kwa mazoea, fuatilieni viongozi wanaokula kiapo kama wanafanyakazi kwa mujibu wa viapo vyao, tokeni nje ya ofisi zenu ili mjue ukweli na uwongo wa maisha ya viongozi,”alisema.

Mhe. Mwanjelwa amesisitiza kuwa kazi nzuri ya kiongozi wa umma inatakiwa kuendana na maadili mema, lakini hatakama kiongozi anafanyakazi nzuri kiasi gani, kama vitendo vyake ni vya hovyo na kiongozi husika ni hovyo.

Awali Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji (Mst) Harold Nsekela wakati akitoa taarifa ya ofisi yake,alimweleza Naibu Waziri kuwa ofisi yake imeanzisha mchakato wa ujazaji wa FomuzaTamko la Rasilimali na Madeni kwa viongozi wa Umma kwa njia ya mtandao.

“Mfumo huu unalengo la kuwasaidia viongozi wa umma zaidi ya elfu 16 kujaza Tamko la Rasilimali na Madeni na kuliwasilisha kwetu wakiwa mahali popote kwa kutumiai TEHAMA bila kufika katika ofisi zetu wala kutuma taarifa zao kwa njia nyingine ikiwemo posta,” alisema.

Kwa mujibu wa Kamishna Nsekela, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma tangu mwaka 2017 imezindua matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa menejimenti ya taarifa za kimaadili (EMIS) ili kurahisisha uchambuzi na upatikanaji wa taarifa za kimaadili zinazosaidia katika utoaji wa maamuzi na kuepuka mfumo wa zamani wa kutumia karatasi.

Alisema, “Mfumo wa EMIS unauwezo wa kukusanya, kuchakata, kutunza taarifa na kumbukumbu mbalimbali kuhusu malalamiko ya ukiukwaji wa maadili, na kufanyauchunguzi wa awali wamalalamiko.”