Dkt. Nchimbi: Maadili ni Nguzo pekee kwa Ustawi wa Jamii yeyote ile.


Dkt. Nchimbi: Maadili ni Nguzo pekee kwa Ustawi wa Jamii yeyote ile.
25
Apr
2019

Dkt. Nchimbi: Maadili ni Nguzo pekee kwa Ustawi wa Jamii yeyote ile.

Imelezwa kuwa Maadili ni Nguzo pekee kwa Ustawi wa Jamii yeyote ile.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Dkt. Rehema Nchimbiwakati akifungua Mafunzo ya Maadili kwa Viongozi Waandamizi wa Mkoa wa Singida yaliyotolewa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Kanda ya Kati - Dodoma yaliyofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida Aprili 18, 2019.

Dkt. Nchimbi alieleza kuwa Maadili nisuala la kijamii na kimaisha na ndiyo nguzo pekee kwa jamii yoyote ile ili iweze kustawi na kwamba pasingekuwepoMaadili dunia isingekuwepo na ndiyo maana Mungu alivyoumba dunia akaweka na mfumo wa Maadili.

Kwa mujibu wa Dkt. Nchimbi, Maadili yanaanza na mtu binafsi hivyo aliwaasa Viongozi wenzake kujipima na kujitathmini kwa matendo na mienendo yao kama yanaleta tija kwa taifa katika maeneo wanayofanyia kazi.

Mhe. Dkt Nchimbi alitumia fursa hiyo kuishukuru Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kupitia Ofisi yake ya Kanda ya Kati Dodoma kwa kuwapatia mafunzo ya Maadili Viongozi wa Mkoa wa Singida ili waweze kutimiza majukumu yao kwaweledi na ufanisi kama inavyotakiwa na Misingi ya Maadili iliyowekwa kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995.

“Tumefarijika sana kwa ujio wenu ambao umelenga kuja kutufundisha, kutukumbusha na kutupima. Ujio huu ni wa faraja kubwa sana na niseme kwamba mnatutakia mema.” Alibainisha Mhe. Dkt Nchimbi.

Kwaupande wake Kaimu Katibu Msaidizi, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Kanda ya Kati Dodoma Bibi. Jasmin Bakari alieleza kwamba lengo la mafunzo hayo ni kuwakumbusha Viongozi Misingi ya Maadili ili wakaweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi hivyo Serikali iweze kutimiza malengo iliyojiwekea ya kuwaletea maendeleo wananchi pamoja na kukuza imani ya wananchi kwa Viongozi na Serikali yao.

“Lengo letu la kuja hapa ni kuendelea kukumbushana kuleana katika misingi ya Maadili ili tuweze kufanya kazi zetu kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu na hatimaye mwisho wa siku malengo ya sereikali ya kuwapatia huduma bora wananchi pamoja na maendeleo yaweze kufikiwa kikamilifu” Alisema Bibi Jasmin.

Mafunzo hayo yalihusisha uwasilishwaji wa mada mbili ambazo ni Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Mgongano wa Maslahi kwa viongozi waandamizi wa Mkoa wa Singida ambao ni pamoja na Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala Mkoa, Makatibu Tawala Wasaidizi, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Wilaya pamoja na Wakuu wa Idara katika Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Singida.