Jaji Nsekela: Fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni sasa kupatikana mtandaoni tu.


Jaji Nsekela: Fomu za Tamko  la Rasilimali na Madeni sasa kupatikana mtandaoni tu.
13
Nov
2017

Viongozi wa Umma waliotajwa na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma sasa watalazimika kuzitafuta Fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni wenyewe kwa kuzipakua (download) kupitia tovuti ya Sekretarieti ya Maadili.

Tamko hilo limetolewa na Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji (Mst.) Harold Nsekela wakati alipomtembelea Ofisini kwake Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martin Shigela hivi karibuni, jijini Tanga.

Mhe. Nsekela alisema kuwa kuanzia mwaka huu 2017 Sekretarieti ya Maadili haitowajibika kuwasambazia Fomu hizo viongozi na kwamba viongozi wenyewe ndio wanaowajibika kuzitafuta kwa kuzipakua kupitia tovuti ya Sekretarieti ya Maadili ambayo ni www.ethicssecretariat.go.tz na tovuti ya serikali ambayo www.tanzania.go.tz.

“Kama kuhamasishana imefikia mwisho na hata Sheria inamtaka kiongozi wa umma kujaza Fomu ya Tamko na kuiwasilisha kwa Kamishna wa Maadili na sio vyenginevyo” alifafanua Mhe. Nsekela.

Kuhusu usimamizi wa Maadili ya viongozi wa umma nchini, Jaji Nsekela alimueleza Mkuu wa Mkoa kuwa kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa viongozi wa umma kwamba Sekretarieti ya Maadili inawasumbua viongozi hususani kuhusu ujazaji wa Fomu za Tamko. Aidha Mhe. Nsekela alifafanua kuwa ni vema viongozi wa umma wakaelewa kuwa Sekretarieti ya Maadili inafanya hivyo kwa ajili ya kutekeleza Sheria.

“Hata mimi mwenyewe ninajaza Fomu hizo na kuziwasilisha kwa Mhe. Rais. Sekretarieti ya Maadili inafanya hivyo kwa ajili ya kutekeleza wajibu wake wa kisheria na ninakuomba Mhe. Mkuu wa Mkoa uwaeleze walio chini yako kuhusu hilo” alifafanua Mhe Nsekela.

Jaji Nsekela aliendelea kumueleza Mhe. Mkuu wa Mkoa kuwa kutoa Tamko la Rasilimali na Madeni sio jambo la hiari, ni wajibu wa kisheria ambao hata Mhe. Rais huwa anafuatilia kwa karibu. Mhe.Nsekela alitumia fursa hiyo pia kuwaomba viongozi wa umma kujaza fomu hizo kwa uaminifu mkubwa kwani kuna athari za kujaza fomu hizo kwa haraka haraka.

Kwa mujibu wa Kamishna wa Maadili, Sekretarieti ya Maadili ina wajibu wa kisheria wa kufanya uhakiki wa Fomu hizo baada ya kujazwa na kwamba msingi wa zoezi la uhakiki unaanzia kwenye Fomu za Tamko.

Mhe. Nsekela aliendelea kubainisha kuwa kiongozi wa umma anatakiwa kutoa maelezo juu ya mali aliyoipata kwa kutaja chanzo chake. Aidha, kuhusu malengo ya kufanya uhakiki, Mhe. Nsekela alisema kuwa lengo la kufanya uhakiki ni kujua kama mali ya kiongozi ameipata kihalali au la pamoja na kuepusha uwezekano wa kiongozi kuficha mali.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martin Shigela alimueleza Kamishna wa Maadili Mhe. Harold Nsekela kuwa ameyapokea maelekezo yake na kumuahidi kuyafanyia kazi. Aidha, Mhe. Shigela alimpongeza Kamishna wa Maadili kwa utaratibu mpya wa ujazaji wa Fomu za Tamko la Rasimali na Madeni na kumuahidi kuwaeleza walio chini yake kwa ajili ya utekelezaji wa wajibu huo wa kisheria.

“Maadili sio tu mali umepataje lakini ni suala la maisha kwa ujumla ya kiongozi ikiwemo matumizi mazuri ya madaraka” alifafanua Mhe. Shigela.

Mhe. Shigela alimuahidi Kamishna wa Maadili kuwa ataendelea kutoa ushirikiano katika kutekeleza majukumu hayo ya kisheria na kwamba atakuwa anawakumbusha viongozi walio chini yake.

Kamishna wa Maadili Mhe. Harold Nsekela alifanya ziara ya siku moja Mkoani Tanga ambapo pamoja na mambo mengine, alifungua mafunzo ya Makatibu Mahsusi, Watunza Kumbukumbu na Wasaidizi wa Ofisi wa Sekretarieti ya Maadili. Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo katika Utunzaji na Usimamizi wa Mifumo ya Taarifa, ikiwa ni sehemu ya Mradi Mkubwa wa Kujenga Uelewa kwa Umma kuhusu Shughuli zinazotekelezwa na Sekretarieti ya Maadili unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani USAID.