Kamishna Nsekela: Zingatieni mgongano wa Maslahi mnapojadili rasimu ya kanuni


Kamishna Nsekela: Zingatieni mgongano wa Maslahi mnapojadili rasimu ya kanuni
29
Jan
2018

Kamishna Nsekela: Zingatieni mgongano wa Maslahi mnapojadili rasimu ya kanuni

Kamishna wa Maadili Jaji (Mst) Harold Nsekela amewataka wadau wa maadili kuzingatia suala la mgongano wa maslahi wanapojadili rasimu ya kanuni za maadili ili kupata kanuni sahihi zitakazosaidia kutekeleza Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na 13 ya mwaka 1995.

Kamishna Nsekela alisema hayo mwishoni mwa wiki mjini Dodoma wakati akifungua warsha ya wadau kujadili kanuni za Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

“Ndugu washiriki wa warsha hii tuweke msisitizo katika sualal la mgongano wa maslahi na kutoa mapendekezo kwani suala lhili ni gumu sio tu kwa Tanzania bali pia nchi nyingine zinazoendelea,” alisema.

Kamishna Nsekela aliwataka washiriki hao kujadili kanuni kwa kujenga msingi thabiti utakaosaidia kuongeza uadilifu miongozi mwa viongozi wa umma ili kuepuka udanganyifu hasa katika kutoa Tamko la Rasilimali na Madeni.

“Tunapojadili kanuni hizi, naomba tujadili kwa kuzingatia matakwa ya Katiba ya nchi na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995 ili kupata kanuni sahihi za utekelezaji wa Sheria,” aliongeza.

Mjadala wa kujadili rasimu ya kanuni za maadili unatokana na ukosefu wa kanuni zilizopitishwa kutafsiri Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma tangu ilipotungwa mwaka 1995.

Uwepo wa kanuni za maadili utatoa fursa kwa wananchi kupata ufafanuzi juu ya tabia, mienendo ya viongozi na matumizi mabaya ya madaraka katika utendaji wao wa kazi.

Baadhi ya wadau walioudhuria warsha hiyo iliyofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ni viongozi wa dini, vyama vya siasa, wawakilishi kutoka asasi za kiraia na wabunge.