Kamishna wa Maadili akiongoza kiapo cha Uadilifu kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani na Jaji Kiongozi.


Kamishna wa Maadili akiongoza  kiapo cha Uadilifu kwa  Majaji wa Mahakama ya Rufani na Jaji Kiongozi.
05
Jun
2018

Kamishna wa Maadili ya Viongozi wa Umma Jaji (Mst) Halord Nsekela Juni 4,2018 ameongoza kiapo cha uadilifu kwa majaji wawili wa Mahakama ya Rufani na Jaji Kiongozi, walioteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.

Majaji wa Mahakama ya Rufani walioapishwa ni Jaji Ferdinand Leons Wambali na Jaji Mwanaisha Athumani Kwariko na Jaji Dkt. Elieza Mbuki Fereshi aliyeteuliwa kushika wadhifa wa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Hafla ya kiapo hicho imefanyika Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya Rais Magufuli kuwaapisha kushika nyadhifa zao mpya.

Hafla hiyo imeudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassimu Majaliwa Majaliwa, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi na wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama.

Wakizungumza mara baada ya kuapishwa na Mhe. Rais, Majaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Wambali na Mhe. Kwariko wamemshukuru Mhe. Rais kwa imani kubwa aliyoionyesha kwao nakuahidi utumishi uliotukuka kwa kutoa haki kwa watu wote.

Kwa upande wake Jaji Kiongozi amemhakikishia Mhe. Rais kuwa atazingatia maadili katika utendaji wake wa kazi.

“Mhe. Rais napenda kukuhakikishia kuwa katika utendaji wangu wa kazi, nitazingatia maadili pamoja na watu ninaowasimamia ili wawe mfano kwa viongozi wengine,” amesema.

Mhe. Fereshi pia ameahidi kusimamia vizuri mpango wa uboreshaji wa mfumo wa mahakama ikiwa ni pamoja na kukabiliana na mrundikano wa kesi na kutoa wito kwa wadau wengine wa mahakama kuendana na kasi ya mahakama kuboresha mifumo yao.

Wadau wa Mahakama ni pamoja na Magereza, Jeshi la Polisi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi wa Mashtaka na Mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai.