Kamishna wa Maadili awaasa Wasanii nchini kubuni Tungo zenye Ujumbe kuhusu Maadili ya Viongozi wa Umma.


Kamishna wa Maadili awaasa Wasanii nchini kubuni Tungo zenye Ujumbe kuhusu Maadili ya Viongozi wa Umma.
07
Nov
2018

Kamishna wa Maadili Mhe. Harold Nsekela amewaasa Wasanii wa fani mbalimbali nchini kubuni tungo zenye ujumbe kuhusu maadili ya Viongozi wa Umma na umuhimu wake kwa jamii ya watanzania.

Rai hiyo imetolewa na Katibu, Idara ya Ukuzaji wa Maadili Bw. Waziri Kipacha wakati akisoma hotuba ya ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo Wasanii kuhusu Maadili ya Viongozi kwa niaba ya Kamishna wa Maadili Mhe. Harold Nsekela yaliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) mjini Morogoro Novemba 6, 2018.

Mhe. Nsekela aliwahamasisha wasanii hao kutumia ushawishi wa sanaa kuwa walimu wa kuifundisha jamii maadili kwa vielelezo na mifano ya mambo maovu ambayo jamii haipaswi kuyafuata kwa kuwa ni kinyume cha maadili ya jamii ya watanzania.

“Naamini mnaweza kutumia na kubuni sanaa za mitindo ya aina mbalimbali kama vile nyimbo, ngoma, mashairi kwa lugha ya kawaida yenye ufasaha ambayo inaeleweka kwa mwananchi wa kawaida.Ninyi ni sehemu ya jamii yetu, mnaishi katika jamii na mnaelewa nini kinafaa kwa wanajamii wenzenu” alifafanua Mhe. Nsekela.

Pia, Mhe.Nsekelaalitumia fursa hiyo kuwatahadharisha Wasanii kuepuka kubuni tungo zenye muelekeo wa kukashifu jamii au serikali na badala yake wajikite kubuni tungo zenye maudhui mema yanayowahusu wananchi katika kupiga vita umaskini, ujinga na maradhi na kuhimiza utawala bora ili kufikia malengo hayo.

Kuhusu Mgongano wa Maslahi, Mhe. Nsekela alisema kuwa tatizo la Mgongano wa Maslahi lina athari kubwa kwa maendeleo ya nchi kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.

Mhe. Nsekela aliongeza kusema kuwa Mgongano wa Maslahi hutokea pale ambapo kiongozi mwenye dhamana anapofanya maamuzi na kutumia nafasi yake kwa maslahi yake binafsi au ndugu, jamaa ama rafiki.

Akichangia katika mafunzo hayo Msanii kutoka kikundi cha Kijogoo Bw. Chedleli G. Senzigha alisema kuwa Msanii sio kioo cha jamii bali ni taswira ya jamii.Kazi ya taswira ni kuakisi hivyo aliwaomba wasanii wenzake nchini kuwa waadilifu na kubuni tungo zenye maadili kwa jamii zinazoakisi matatizo yanayoikabili jamii inayowazunguka.

Mafunzo hayo ya siku moja yalilenga kuwajengea uwezo wawakilishi wa vikundi vya sanaa kutoka mikoa ya Dodoma, Iringa, Morogoro na Mtwara ili waweze kutumia sanaa katika kukuza na kusimamia Maadili kwa ujumla.Aidha, mafunzo hayo ya Wasanii ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi mkubwa wa Kujenga Uelewa wa Wananchi kuhusu kazi zinazofanywa na Sekretarieti ya Maadili kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Misaada ya Maendeleo la Watu wa Marekani (USAID).