Kamishna wa Maadili awataka Maafisa Bajeti kukumbuka na kuzingatia majukumu ya Taasisi.


Kamishna wa Maadili awataka Maafisa  Bajeti kukumbuka na kuzingatia majukumu ya Taasisi.
14
May
2019

Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji (Mst.) Harold Nsekela amewataka Maafisa Bajeti wa Sekretarieti ya Maadili kukumbuka na kuzingatia majukumu ya Taasisi iliyopewa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 Ibara ya 132.

Rai hiyo ameitoa wakati akifunga mafunzo ya Maafisa Bajeti kuhusu Tathmini na Ufuatiliaji, Uchambuzi wa Taarifa na Takwimu na Uandishi wa Taarifa zinazoambatana na Takwimu yaliyofanyika Mkoani Morogoro kuanzia tarehe 6-10 Mei, 2019.

Mhe. Nsekela aliyataja majukumu hayo kuwa ni pamoja na Kupokea Hati za Tamko la Rasilimali na Madeni zinazohitajika kutolewa na Viongozi wa Umma kwa mujibu wa Katiba na Sheria, Kupokea malalamiko na taarifa dhidi ya ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma wanaopaswa kuwajibika chini ya Sheria na Kufanya Uhakiki wa Mali na Madeni ya Viongozi wa Umma.

Majukumu mengine ni Kuchunguza tuhuma yoyote ya kuvunjwa kwa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma wanaopaswa kuwajibika chini ya Sheria pamoja na Kuanzisha na kufanya uchunguzi kuhusu ukiukwaji wa Maadili ya Viongozi wa Umma.

Akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo, Mhe. Nsekela alisema kuwa mafunzo hayo yana umuhimu mkubwa kwa washiriki kutokana na jukumu kubwa la kuandaa bajeti za Idara/Vitengo na Ofisi za Kanda. Aidha, Mhe. Nsekela aliongeza kusema kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuandaa taarifa za utekelezaji sambamba na kufanya tathmini ya miradi inayoendeshwa na Ofisi kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo.

“Shughuli zote hizi zinahitaji weledi na umakini wa hali ya juu, kwani taarifa ya utekelezaji inapaswa kuwa ya kina na yenye kutoa taswira halisi ya nini kimefanyika kwenye taasisi, na hatimaye kuleta matokeo chanya ya Taasisi.“Ni wazi kwamba utaalamu mlioupata utawawezesha kufanya shughuli zenu kwa ufanisi, kuandaa taarifa za utendaji kazi zenye tija na zinazopima malengo yaliyowekwa na taasisi kwa ufanisi” alisisitiza Mhe. Nsekela.

Pia, Mhe. Nsekela alisema kuwa hiyo ni fursa adimu kwao hivyo aliwataka washiriki hao watakaporudi katika vituo vyao vya kazi wakatekeleze majukumu yao kwa ufanisi kama walivyofundishwa na Mkufunzi ili waongeze tija katika kutekeleza majukumu yao.

Mafunzo hayo ya siku tano yalilenga kuwajengea uwezo Maafisa Bajeti wa Sekretarieti ya Maadili katika maeneo ya Tathmini na Ufuatiliaji, Uchambuzi wa Taarifa na Takwimu na Uandishi wa Taarifa zinazoambatana na Takwimu chini ya ufadhili wa Shirika la Misaada la Uingereza yaani Department for International Development (DFID).