Kamishna wa Maadili awataka Viongozi wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kujiepusha kupokea zawadi.


Kamishna wa Maadili awataka Viongozi wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kujiepusha kupokea zawadi.
24
Oct
2018

Kamishna wa Maadili Mhe. Harold Nsekela amewataka viongozi wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kujiepusha kupokea zawadi wakati wanapotekeleza majukumu yao.

Wito huo aliutoa wakati akiwaapisha Kiapo cha Uadilifu Viongozi wakuu wa Baraza hilo wakiongozwa na Katibu Mtendaji Dkt. Adolf Babiligi Rutayuga katika Ofisi za Sekretarieti ya Maadili jijini Dar es Salaam.

Mhe. Kamishna alisema kuwa Sekretarieti ya Maadili ipo katika mchakato wa kulifanyia kazi jambo hilo ambapo viongozi wa umma watatakiwa kutamka katika fomu zao zawadi wanazopokea ili kuwapa urahisi Sekretarieti kufuatilia jambo hilo kwa ukaribu zaidi.

Akinukuu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya 1995, kifungu cha 12(2) kinachosema kuwa Kiongozi wa umma pale atakapopokea zawadi yenye thamani inayozidi shilingi 200,000/= atatakiwa kutaja zawadi aliyopokea na thamani yake na kukabidhi zawadi hiyo kwa Afisa Mhasibu wa Ofisi inayohusika ambaye atatoa maagizo kwa maandishi kuhusu matumizi ya zawadi hiyo au jinsi ya kuishughulikia kwa njia nyingine yeyote. Alifafanua Mhe. Nsekela.Hata hivyo Mhe. Nsekela aliwaasa viongozi hao kujiepusha kupokea zawadi kwa namna yeyote ile.

Kuhusu Kiapo cha Uadilifu ambacho aliwaapisha viongozi hao, Mhe. Nsekela aliwaasha viongozi hao kuzingatia vipengele vyote 12 ambavyo walikiri mbele yake na kwamba hizo ni taratibu za ajira zao na sio mageni katika utumishi wa umma.Aidha, Mhe. Nsekela aliwataka viongozi hao kujiepusha kutumia vibaya madaraka yao na badala yake wafanye kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zinazowaongoza.

Pia, Mhe. Nsekela aliwakumbusha viongozi hao kutoa Matamko ya Rasilimali na Madeni yao, ya Wenza wao pamoja na Watoto wao ambao wana umri chini ya miaka 18 kwa mujibu wa Sheria.Sambamba na hilo, Kamishna wa Maadili alitumia fursa hiyo kuwaomba wenza wa viongozi hususani wanaume kutoa ushirikiano wakati wa zoezi la uhakiki wa Rasilimali na Madeni ya Viongozi linapofanyika.

Viongozi wengine walioapishwa Kiapo cha Uadilifu na Kamishna wa Maadili ukiacha Dkt. Adolf Babiligi Rutayuga ambaye ni Katibu Mtendaji wa Baraza hilo ni Mkurugenzi wa Habari, Utafiti na Mipango Dkt Marcelina Aloyce Baitilwake na Mkurugenzi wa Ushauri na Usaidizi wa Vyuo vya Ufundi Mhandisi, Dkt. Gemma Kishari Modu.