Kamishna wa maadili azindua Awamu ya Pili ya urushaji vipindi vya Elimu ya Maadili


Kamishna wa maadili azindua Awamu ya Pili ya urushaji vipindi vya Elimu ya Maadili
30
Jul
2018

Kamishna wa Maadili Jaji (Mst) Harold Nsekela amezindua awamu ya pili ya program ya urushaji wa vipindi vya kutoa Elimu ya Maadili kwa umma katika mikoa ya Morogoro na Iringa huku akisisitiza kuwa lengo la vipindi hivyo ni kuimarisha mawasiliano kati ya wananchi na Sekretarieti ya Maadili kupitia redio za kijamii.

Uzinduzi huo ulifanyika kupitia redio Planet ya mkoani Morogoro na NURU FM ya Iringa,mwishoni mwa wiki.

Awamu ya kwanza ya program ya urushaji vipindi vya Elimu ya Maadili ilizinduliwa mwaka 2013. Mradi huo wa utoaji wa Elimu ya Maadili kwa umma unafadhiliwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la watu wa Marekani (USAID).

Kamishna Nsekela alisema kuwa mawasiliano yatakayoimarishwa kupitia vipindi hivi ni yale yanayohusiana na mamlaka ya kisheria ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995.

Alisema, “lengo la mradi huu ni kuimarisha mawasiliano kati ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na wananchi kuhusu kazi na mamlaka ya kisheria ya Sekretarieti ya Maadili, maadili ya viongozi kwa mujibu wa sheria ya Maadili, na kukumbushana wajibu wa wananchi na wadau mbalimbali katika ukuzaji na usimamizi wa maadili ya viongozi.”

Kwa mujibu wa Kamishna Nsekela, katika awamu ya pili, vipindi vya rediovimeongezeka kutoka 10 vilivyorushwa katika awamu ya kwanza hadi 26. Nyongeza hii itasaidia wananchi kupata fursa ya kuuliza na kujibiwa maswali yao, kutoa maoni na mapendekezo kuhusu maadili ya viongozi.

Alisema, kupitia vipindi vilivyorushwa katika awamu ya kwanza imebainika kwamba kuna ongezeko la uelewa wa wananchi kuhusu maadili ya viongozi na majukumu yanayotekelezwa na Sekretarieti ya Maadili ya viongozi wa Umma.

“Pamoja na ongezeko hilo, bado elimu zaidi inahitajika kuwafikia wananchi wengi hususani wanawake ambao ushiriki wao katika vipindi vya awali ulikuwa mdogoikilinganishwa na wanaume,” amesema.

Vipindi hivyo pia vinarushwa katika mikoa ya Dodoma, Mtwara, na Dar es Salaam.

Jaji Nsekela alisema kuwa Maadili ya Viongozi ni nyenzo muhimu ya kukuza utawla bora nchini. “Maadili ndiyo msingi wa maendeleo ya kiuchumi, kijamii, kisiasa, na kiutamaduni, uongozi bora na Maadili unapaswa kuwa mfumo wa jamii zetu ili tuweze kufikia maendeleo endelevu,” amesema.

Kamishna wa Maadili amesema, “Ili tuweze kufanikisha matarajio ya dira ya Maendeleo, ni muhimu wananchi wajengewe uwezo wa kusimamia uwajibikaji wa Viongozi na Watumishi wa umma.

Kwa mujibu wa Kamishna wa Maadili, vipindi hivi vitawajengea uwezo wananchi wa kushirikiana na Sekretarieti ya Maadili kukuza na kusimamia maadili hapa nchini.”