Maafisa Bajeti wa Sekretarieti ya Maadili wapatiwa Mafunzo kuhusu Ufuatiliaji na Tathmini pamoja na Uandishi wa Taarifa.


Maafisa Bajeti wa Sekretarieti ya Maadili wapatiwa Mafunzo kuhusu Ufuatiliaji na Tathmini pamoja na Uandishi wa Taarifa.
07
May
2019

Katika kuboresha utendaji kazi wa majukumu yao, Uongozi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma umewaandalia mafunzo ya Siku tano Maafisa Bajeti wake kutoka Idara, Vitengo na Ofisi za Kanda yanayofanyika Mkoani Morogoro kuanzia tarehe 6 – 10 Mei, 2019.

Akifungua mafunzo hayo Afisa Rasilimaliwatu Mwandamizi Bw. Suleiman Madega ambaye alimwakilisha Kamishna wa Maadili katika ufunguzi wa Mafunzo hayo, alisema kuwa chimbuko la mafunzo hayo limetokana na mapungufu yaliyojitokeza katika uandishi wa taarifa zao hususani za utekelezaji katika Idara, Vitengo na Kanda.

Bw. Madega aliyataja baadhi ya mapungufu hayo kuwa ni pamoja na taarifa nyingi kukosa takwimu hivyo kuondoa kiungo muhimu katika uandishi wa taarifa za taasisi.

“Ni vigumu kuwaleta hapa watumishi wote kupewa mafunzo haya, hivyo ni muhimu baada ya mafunzo haya kwenda kuwafundisha wenzenu waliobaki ofisini.Na hii isiwe kwenye mafunzo haya tu bali ni kwa kila mafunzo ambayo mtakuwa mmehudhuria ili kuboresha utendaji kazi wenu wa kila siku”. alibainisha Bw. Madega.

Naye Mwezeshaji wa mafunzo hayo Bw. Apronius Mbilinyi alisema kuwa mafunzo hayo yatakuwa shirikishi na kwamba yatajikita katika maeneo mengi kama vile matumizi ya takwimu katika uandishi wa taarifa kwa kuzingatia Mpango Mkakati wa Taasisi.

Kwa mujibu wa ratiba ya mafunzo hayo, kutakuwa na mada mbalimbali ambazo zitafundishwa katika kipindi cha siku tano ambazo ni pamoja na Kuandaa Viashiria, Shabaha wakati wa kufanya Ufuatiliaji na Tathmini, namna ya kufanya Ufuatiliaji na Tathmini katika Sera na Mpango Mkakati na namna ya kuchakata Data kwa kutumia Program ya “SPSS and Advanced Excel”.

Mafunzo hayo ni ya pili kufanyika kwa maafisa hao, ambapo mafunzo kama hayo yaliwahi kufanyika mwaka 2018 mkoani Mtwara ambapo yalisaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha utendaji kazi hususani uandishi wa taarifa za robo mwaka za Taasisi.