Mahakimu Wanawake Dar es Salaam watakiwa Kuzingatia Maadili wakati wa utoaji Haki Mahakamani.


Mahakimu Wanawake Dar es Salaam watakiwa Kuzingatia Maadili wakati wa utoaji Haki Mahakamani.
23
Oct
2018

Mahakimu Wanawake wa Mkoa wa Dar es Salaam wametakiwa kuzingatia Maadili katika utoaji haki ili kulinda heshima ya Waheshimiwa Mahakimu machoni pa watu na kulinda matumaini na imani ya wananchi kwa mhimili wa Mahakama.

Wito huo umetolewa na Naibu Msajili wa Mahakama, Kanda ya Dar es Salaam Mhe. Joackim Tiganga wakati akifungua Mafunzo ya Maadili kwa Mahakimu Wanawake wa Mkoa wa Dar es Salaam yaliyoandaliwa na Sekretarieti ya Maadili na kufanyika katika ukumbi wa Ofisi Ndogo za Bunge, jijini Dar es Salaam.

Mhe. Tiganga alisema kuwa Mahakama ya Tanzania iko kwenye kampeni kubwa ya kuhubiri na kusimamia maadili kwa viongozi na watumishi wake.Mafunzo haya yamekuja wakati muafaka na hii ni ishara kwamba maadili sasa ni wimbo wa kila taasisi ya umma hasa kwa viongozi, alifafanua Mhe Tiganga.

“Tusipotenda haki katika maamuzi tunayofanya tunasababisha watu kujichukulia sheria mkononi, hivyo tutasababisha utovu wa maadili kwa wananchi wa kawaida ambao siyo hulka yao kuwa hivyo. Kutenda haki kunasaidia kujenga maadili katika jamii pamoja na kudumisha amani”. Alisema Mhe. Tiganga.

Akizungumzi kuhusu tatizo la mgongano wa maslahi, Mhe. Tiganga alisema kuwa suala hili ni nyeti na pana sana. Mhe. Tiganga aliendelea kufafanua kuwa ni vema kuchukuwa tahadhari kubwa katika eneo hili na kueleza kuwa si Tanzania pekee ambayo inakabiliana na changamoto ya tatizo hili bali ni ulimwengu mzima hata nchi kubwa zilizoendelea nazo zinakabiliwa na changamoto hii.

“Tatizo hili la Mgongano wa Maslahi lina athari kubwa kwa maendeleo ya nchi kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.Mgongano wa Maslahi hutokea pale ambapo kiongozi mwenye dhamana anapofanya maamuzi na kutumia nafasi yake kwa maslahi yake binafsi au ndugu, jamaa ama rafiki.Unapofanya maamuzi kwa kulinda maslahi ya mtu fulani basi ujue kuwa umejiingiza katika Mgongano wa Maslahi” Alisisitiza Mhe. Tiganga.

Akifunga mafunzo hayo, Katibu – Idara ya Usimamizi wa Maadili katika Sekretarieti ya Maadili Bw. John Kaole alisema kuwa bado kuna matatizo ya kimaadili katika mihimili yetu ya dola na jamii hapa nchini kwa ujumla.

Kwa mujibu wa Bw. Kaole hali hiyo inatokana na utoaji huduma usioridhisha, migongano ya maslahi, matumizi mabaya ya madaraka, wizi na ubadhirifu wa mali za umma, unyanyasaji wa kijinsia, kujilimbikizia mali isivyo halali, rushwa, upendeleo, unyanyasaji wa kijinsia, kutozingatia Sheria na Kanuni, maamuzi yasiozingatia haki, chuki na uchochezi wa kiitikadi, kukosekana kwa uzalendo, matumizi ya lugha chafu na ukiukwaji wa maadili ya kitaaluma.

Bw. Kaole aliendelea kufafanua kuwa sifa njema ya Mahakama inalindwa na Majaji, Mahakimu na Watumishi wa mahakama wanaotekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kwa kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni, Miongozo ya Kisheria, Mila na Desturi za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mafunzo hayo ya siku moja kwa Mahakimu Wanawake wa Mkoa wa Dar es Salaam yamefadhiliwa na Shirika la USAID na ni mwendelezo wa Mkakati wa Sekretarieti ya Maadili wa kuwafikia Viongozi wote wa umma ili kuwapa elimu kuhusu maadili ya viongozi.