Makamu Wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan Atangaza Kuwa Uhakiki Wa Vyeti Ni Zoezi Endelevu Katika Utumishi Wa Umma


Makamu Wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan Atangaza Kuwa Uhakiki Wa Vyeti Ni Zoezi Endelevu Katika Utumishi Wa Umma
13
Dec
2017

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewaonya watumishi wenye vyeti feki waliosalimika akisema awamu ya pili inakuja.

Akizungumza katika ufunguzi wa kilele cha maadhimisho ya siku ya Maadil Duniani kwenye viwanja vya Nyerere Square Mjini Dodoma akisema kutokana na kutoridhisha na utendaji kazi wa baadhi ya Taasisi, Serikali imeamua kufuatilia idadi halali ya watumishi wa umma, uhalali wa vyeti na ulipaji wa mishahara. Mhe. Samia Suluhu Hassan alisema, “Kazi hii itakuwa endelevu Ndugu zangu, kama kuna mtu aliyenusurika wimbi la kwanza naomba akae vizuri wimbi la pili linakuja. Serikali imekuwa ikipoteza fedha kutokana na watumishi hewa, jambo hili hatuwezi kulifumbia macho. Serikali haiwezi kuendelea kuwa na watumishi hewa, wasiowajibika na wasiofanya kazi kikamilifu au kufanya kazi kwa ugoigoi”.

Akizungumzia utendaji Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan alisema, katika kutatua changamoto za utumishi, Serikali imeanza kuweka mfumo wa kanzi data na mifumo ya kutoonana wakati wa kutoa huduma. Pia kuna tabia ya baadhi ya watumishi wa Serikali kufanya kazi bila kupata mikataba ya huduma kwa wateja. Ni vyema huduma zinazotolewa zikaainishwa bayana na muda utakaotumika.

Vilevile kama kuna mtu mzembe mahali popote nawataka viongozi wasisite kumuondoa hakutakuwa na mapengo mengi katika ajira. Kuna vijana wengi wanasubiri ajira ambao tutataka tuwajengee uzalendo, ubunifu na uadilifu mkubwa. Kuna kesi nyingi katika mahakama ya kazi zinazohusu ukosefu wa maadili kwa vijana, wizi na kutowajibika. Hatuwezi kusema tunajenga Tanzania ya uchumi wa kati kama vijana wako kwenye njia hii ya maisha.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Mkuchika alisema, katika mapambano dhidi ya rushwa, kuelimisha inachukua nafasi kubwa kwa sababu Watanzania wakielimishwa kuhusu maadili na rushwa kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu tatizo la ukosefu wa maaadili litapungua kwa kaisi kukubwa. “Tuanze na wafanyakazi wa Serikali, leo kuna mkutano wa Baraza la wafanyakazi, tunaomba mkiwa na mikutano kama hiyo mtualike kuja kutoa semina” alisema.

Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali Ndugu George Masaju alisema, hivi karibuni yamejitokeza madai kama vile haki ya ndoa za jinsia moja. “Ukweli ni kwamba hiyo ndiyo haki hatarishi dhidi ya binadamu kwa sababu watu watakosa fursa ya kuzaliana na hii ndio itakwenda kuua taifa kwani binadamu hawatakuwepo” alisema.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai (Mb.) alisema Bunge liko tayari katika kutunga au kurekebisha sheria utungaji kwa lengo la kutilia mkazo na kuboresha maadili ndani ya nchi.

Jumla ya Taasisi 10 za Umma zilishiriki katika Maadhimisho ya siku ya Maadili na Haki za Binadamu Nchini. Taasisi hiozo ni Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Tume ya Utumishi wa Umma, TAKUKURU, Ofisi ya Taifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali-NAOT, PPRA, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Jeshi la Polisi.