Mapambano dhidi ya Rushwa na Ufisadi yatafanikisha Azma ya Uchumi wa kati wa Viwanda Nchini.


Mapambano dhidi ya Rushwa na Ufisadi yatafanikisha Azma ya Uchumi wa kati wa Viwanda Nchini.
07
Dec
2017

Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Mhe. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria kwa dhati kuifikisha nchi yetu katika Uchumi wa Kati na kwamba hakuna nchi inayoweza kuleta mabadiliko ya kiuchumi bila kupambana na rushwa na ufisadi.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Dodoma Bw. Emmanuel Kuboja ambaye alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa wiki ya kutoa huduma kwa Umma katika kuadhimisha siku ya Maadili na Haki za Binadamu kItaifa iliyofanyika katika Viwanja vya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Mkoani Dodoma.

Aidha Bw. Kuboja katika hotuba yake amebainisha kwamba suala la Maadili ni mtambuka kwakuwa linamgusa kila mtanzania na ametoa wito kwa Taasisi zote za Umma na Sekta Binafsi na makundi mbalimbali katika Jamii kuwa chachu ya kuliwezesha taifa kutekeleza na kusimamia Uwajibikaji, Uadilifu, Haki za Binadamu, Utawala Bora na Mapambano Dhidi ya Rushwa.

Bwana Kuboja aliongeza kuwa dhumuni kubwa la maadhimisho hayo ni pamoja na kuikumbusha na kuihamasisha jamii kujua haki zao na wajibu wao kama raia na kuwaunganisha wananchi kukusanya nguvu ya pamoja kuhakikisha wanapambana na kukabiliana na changamoto za Maadili, Rushwa na Haki za Binadamu.

Maadhimisho ya siku ya Maadili na Haki za Binadamu kitaifa mwaka huu yamefanyika kwa mara ya kwanza katika Manispaa ya Dodoma ambapo Kauli mbiu ya Maadhimisho hayo ni " Wajibika: piga Vita Rushwa, zingatia Maadili, Haki za Binadamu na Utawala Bora, kuelekea Uchumi wa Kati".

Maadhimisho hayo yameshirikisha jumla ya Taasisi za Umma ambazo ni Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma,TAKUKURU, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Tume ya Utumishi wa Umma, Mamlaka ya Manunuzi ya Umma, Tume ya Haki za Binadamu , Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Jeshi la Polisi