Mhe. Nsekela: Uadilifu ni Sharti ujengwe ndani ya Jamii.


Mhe. Nsekela: Uadilifu ni Sharti ujengwe ndani ya Jamii.
16
Jul
2018

Uadilifu ni sharti ujengwe ndani ya jamii ili uwe sehemu ya utamaduni wa nchi.

Kauli hiyo imetolewa na Kamishna wa Maadili Mhe. Harold Nsekela wakati akifungua Semina kwa Waheshimiwa Madiwani na Wakuu wa Idara Wanawake kutoka Manispaa za Mkoa wa Dar es Salaam kuhusu Maadili ya Viongozi wa Umma kwenye Ukumbi wa Anautoglou jijini Dar es Salaam.

Mhe. Nsekela alifafanua kuwa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Kanuni za Serikali za Mitaa pamoja na Vyombo vya Kusimamia Utawala Bora pekee haviwezi kufanikisha suala la kukuza na kusimamia maadili.

“Jukumu la kukuza na kusimamia maadili ya viongozi linahitaji ushirikiano wa pamoja kati ya viongozi, wananchi na wadau mbalimbali” alibainisha Mhe. Nsekela.

Akielezea sababu za kuandaa mafunzo hayo kwa viongozi wanawake pekee Mhe. Nsekela alisema kuwa chimbuko na kiini hasa cha mafunzo hayo ni matokeo ya utafiti uliofanyika Oktoba, 2015 uliokuwa unapima ushiriki wa utoaji wa taarifa uliofanywa na makundi mbalimbali katika jamii kuhusu ukiukwaji wa Maadili miongoni mwa viongozi wa umma.

Mhe. Nsekela aliendelea kusema kuwa matokeo ya utafiti huo yalionesha kuwa ni asilimia moja (1%) tu ya wanawake kwenye vijiji na Mitaa walishiriki katika kutoa taarifa za uikukwaji wa Maadili.

Kwa mujibu wa Mhe. Nsekela hali hiyo iliilazimu Sekretarieti ya Maadili kuandaa mafunzo hayo katika Mikoa inayotekeleza Mradi wa Kukuza Uelewa wa Wananchi kuhusu Majukumu na Kazi zinazotekelezwa na Sekretarieti ya Maadili ambayo ni Mtwara, Morogoro, Iringa, Dodoma na kuijumuisha Dar es Salaam kutokana na umuhimu wake.

Kuhusu umuhimu wa Viongozi wanawake katika jamii Mhe. Nsekela alifafanua kuwa Viongozi wanawake wana ushawishi mkubwa katika jamii hivyo wanapaswa kuongoza katika juhudi za mapambano dhidi ya vitendo vya ukiukaji wa Maadili.

“Hatuna budi kuwahamasisha wananchi kuchukia vitendo vya ukiukaji maadili na kuwakataa viongozi wasio waadilifu.Ni matumaini yangu kuwa elimu mtakayoipata katika semina hii mtaitoa pia kwa wanawake wengine katika Halmashauri zenu, wananchi katika Kata zenu naMitaa ambako mnatekeleza majukumu yenu ya kila siku” alibainisha Mhe. Nsekela.