Mkuchika awataka Watumishi wa Sekretarieti ya Maadili Kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu.


Mkuchika  awataka  Watumishi  wa Sekretarieti ya Maadili Kuzingatia  Sheria, Kanuni na Taratibu.
13
Feb
2018

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Mkuchika (Mb) amewataka watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu wakati wanapotekeleza majukumu yao na kuwa mfano wa kuigwa na watumishi wengine wa serikali.

Kauli hiyo aliitoa hivi karibuni wakati alipofanya ziara iliyokuwa na lengo la kujitambulisha katika Ofisi za Sekretarieti ya Maadili, Makao Makuu jijini Dar es Salaam.

Mhe. Mkuchika aliwatahadhalisha wafanyakazi hao kutoipaka matope taasisi hiyo muhimu ya serikali kwa kujihusisha na mienendo isiyofaa ikiwemo rushwa kwani kazi wanayoifanya ni nyeti na inapaswa kufanywa kwa weledi na umakini wa hali ya juu .

“Taasisi hii hushughulika na Viongozi wa ngazi mbalimbali ambao wengi wao wana maovu yao mengi ambayo watataka yasijulikane hivyo basi watatumia njia yeyote ile ili kufanya kazi kwa matakwa yao” alitahadhalisha Mhe. Mkuchika.

Aidha, Mhe Waziri aliongeza kuwa wakati wa zoezi la uhakiki wa mali na madeni ya viongozi ni wakati mgumu sana kwa watumishi kwani baadhi ya viongozi ambao sio waadilifu wanaweza kutumia fursa hiyo kuwashawishi kupokea rushwa ili kuficha ukweli juu ya mali anazomiliki hivyo kukwamisha jitihada za Serikali ya Awamu ya tano ya kupambana na rushwa.

Kuhusu hali ya Utawala Bora nchini, Mhe. Mkuchika alisema kuwa kwa sasa ni nzuri. Mhe. Mkuchika alibainisha kuwa kwa mujibu wa matokeo ya utafiti wa TWAWEZA yaliyotolewa mwaka jana yanaonesha kuwa vitendo vya rushwa nchini vimepungua.

Kuhusu elimu kwa umma, Mhe. Waziri aliipongeza Sekretarieti ya Maadili kwa kufanya kazi nzuri ya kutoa elimu kwa Umma kupitia vyombo vya habari na Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu yanayofanyika Desemba 10 ya kila mwaka. Aidha, Maadhimisho hayo kwa mwaka jana yalifanyika Makao Makuu ya nchi Dodoma.

Awali akimkaribisha Mhe. Waziri, Kamishna wa Maadili Mhe. Harold Nsekela alisema kuwa kwa sasa viongozi wa umma wanapakua (download) Fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni kwenye tovuti ya Sekretarieti ya Maadili yaani www.ethicssecretariat.go.tz jambo ambalo limesaidia kupunguza gharama za ofisi na kuwarahisishia Viongozi kuzipata Fomu hizo na kuzijaza kwa wakati ili kukidhi mataka ya Sheria.

Mhe. Kamishna aliongeza kuwa kwa sasa taasisi hiyo iko kwenye mchakato wa kuwawezesha Viongozi hao kujaza Fomu za Tamko kwenye mtandao (online) jambo ambalo litasaidia kurahisisha utendaji kazi wa Sekretarieti ya Maadili.

Mhe. Mkuchika alifanya ziara hiyo iliyokuwa na lengo la kujitambulisha katika taasisi hiyo iliyo chini ya Wizara yake tangu alipoteuliwa na Mhe. Rais kushika wadhifa huo miezi minne iliyopita.