Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya pata ugeni kutoka Botswana.


Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya pata ugeni kutoka Botswana.
26
Jul
2017

Mkurugenzi Mkuu wa Kurugenzi ya Rushwa na Makosa ya Kiuchumi wa Botswana (Directorate on Corruption and Economic Crime) Bi Rose Seretse na ujumbe wake hivi karibuni wamefanya ziara ya siku moja nchini kujifunza jinsi Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma inavyofanya kazi.

Ziara hiyo ilikuwa na lengo la kujua namna viongozi wa umma wanavyotoa matamko yao ya Rasilimali na Madeni pamoja na zoezi la uhakiki wa rasilimali na madeni ya viongozi wa umma linavyofanyika nchini.

Akielezea namna viongozi wa Umma wanavyotoa Matamko yao ya Rasilimali na Madeni, Katibu wa Idara ya Viongozi wa Siasa kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Bw. Waziri Kipacha alisema kuwa Viongozi wote wa Umma waliotajwa na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma wanatakiwa kutangaza mali zao, za wenza wao pamoja na watoto wao wenye umri chini ya miaka 18 katika Fomu maalum na kuiwasilisha kwa Kamishna wa Maadili.

Fomu hiyo inatakiwa kuwasilishwa ndani ya siku thelathini baada ya kushika wadhifa, na kila ifikapo tarehe 31 Desemba ya kila mwaka, mwisho wa kutumikia wadhifa au baada ya kustaafu.

“Viongozi wa Umma waliotajwa katika kifungu cha 4(1) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995 mara wanaposhika wadhifa wanatakiwa kutaja rasilimali zao zote wanazomiliki, za mwenza wao pamoja na watoto wao wenye umri chini ya miaka 18. Hata hivyo, miaka mingine watakuwa wanataja ongezeko au upungufu wa mali” alifafanua Bw. Kipacha.

Bw. Kipacha aliendelea kuueleza Ujumbe huo kuwa kwa upande wa Wabunge wanatakiwa kujaza Fomu mbili za matamko na kuziwasilisha kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, Spika hubakiwa na nakala moja ya Tamko na nakala nyingine huiwasilisha kwa Kamishna wa Maadili.

Katibu huyo aliueleza ujumbe kutoka Botswana kuwa Kamishna wa Maadili, yeye Tamko lake la Rasilimali na Madeni huliwasilisha kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kuhusu lengo la utaratibu huo Bw. Kipacha aliueleza Ujumbe huo kuwa Viongozi wa Umma kutoa Matamko ya Mali na Madeni yao ni kuwafanya viongozi hao kuzitumia mali hizo bila kuleta mgongano wa maslahi.

Naye Bi Rose Seretse akielezea siri ya mafanikio ya Botswana kuwa na kiwango cha chini cha vitendo vya rushwa barani Afrika, alisema kuwa mafanikio hayo yametokana na mikakati mbalimbali iliyoibuni Taasisi anayoiongoza pamoja na utashi wa kisiasa wa viongozi wakuu wa nchi hiyo wa kupambana na rushwa.

Baadhi ya mikakati iliyobuniwa na taasisi anayoiongoza ni pamoja na kufanya tathmini ya vitendo vya rushwa kwa taasisi za serikali na mashirika ya umma na kutoa alama ya ukubwa wa tatizo la rushwa katika kila taasisi na ripoti ya tathmini hiyo huwasilishwa kwa Rais. Kwa mujibu wa Bi Seretse, Rais huchukua hatua kali kwa viongozi wa taasisi ambazo zimepata alama kubwa kwa vitendo vya rushwa.

Mikakati mingine ni pamoja na uanzishwaji wa vilabu vya kupinga rushwa katika jamii na vijiji, Vilabu vya kupinga rushwa Mashuleni, kuanzisha jukwaa la biashara la Maadili, kuanzisha Kitengo cha Mashtaka/Mahakama ya Rushwa pamoja na kutoa hamasa kwa jamii kuhusu mapambano dhidi ya rushwa nchini humo.