Sekretarieti ya Maadili yajipanga kutumia TEHAMA kutoa huduma zake.


Sekretarieti ya Maadili yajipanga kutumia TEHAMA kutoa huduma zake.
19
Jul
2018

Sekretarieti ya Maadili imejipanga vema katika kuwahudumia Viongozi wa Umma kwa kutoa huduma zenye ufanisi na tija zaidi.

Katika kufikia azma hiyo, katika miaka mitano ijayo, Sekretarieti inajielekeza zaidi katika matumizi ya TEHAMA katika kuwafikia Viongozi wa Umma kuhusu utekelezaji kazi zake zote ikiwemo utoaji wa elimu.

Hayo yamesemwa na Kamishna wa Maadili Mhe. Harold Nsekela wakati akifungua Semina ya Viongozi wa Serikali za Mitaa wa Mkoa wa Dar es Salaam kuhusu Maadili ya Viongozi wa Umma iliyofanyika katika Ukumbi wa Anautoglu jijini Dar es Salaam.

Mhe. Nsekela alifafanua kuwa kwa sasa Sekretarieti inajiandaa kuanza ujazaji wa Tamko kwa njia ya mtandao “online declaration” ambapo itasaidia viongozi kurejesha Fomu zao kwa haraka.Pia, Sekretarieti inadhamiria kufanya uhakiki kwa njia ya mtandao” online verification” ambapo Sekretarieti itajiunganisha na mitandao mingine ya taasisi za umma ili kuweza kupata taarifa mbalimbali kuhusu mienendo na tabia za Viongozi wa Umma kuhusu umiliki wa rasilimali, alibainisha Mhe. Nsekela.

Akizungumzia kuhusu Mgongano wa Maslahi kwa viongozi wa umma Mhe. Nsekela alisema kuwa tatizo la Mgongano wa Maslahi lina athari kubwa kwa maendeleo ya nchi kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.

“Mgongano wa Maslahi hutokea pale ambapo kiongozi mwenye dhamana anapofanya maamuzi na kutumia nafasi yake kwa maslahi yake binafsi au ndugu, jamaa na rafiki.Unapofanya maamuzi kwa kulinda hisia za mtu Fulani basi ujue kuwa kiongozi umejiingiza katika Mgongano wa Maslahi” alisisitiza Mhe. Nsekela.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Ally Hapi akichangia katika semina hiyo aliiomba Sekretarieti ya Maadili kuweka msukumo zaidi ili kuwezesha nchi kuwa na Sera ya Taifa ya Maadili.

Mhe. Hapi alisema kuwa uwepo wa Sera ya Taifa ya Maadili inayoakisi utamaduni wetu itarahisisha usimamiaji wa utekelezaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Mhe. Hapi aliwapongeza Sekretarieti ya Maadili kwa kuandaa semina hiyo kwani imewapa fursa ya kujikumbusha mambo mbalimbali ya maadili na kuwaomba kutoa elimu zaidi ili kuweka bayana dhamira ya kutungwa kwa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Semina hiyo ya Siku moja kwa viongozi hao wa Mkoa wa Dar es Salaam ilikuwa na lengo la kuwajengea uwezo hususani katika maeneo ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Hati ya Ahadi ya Uadilifu na Mgongano wa Maslahi ili kuwawezesha kuwa mabalozi na wasimamizi wazuri katika maeneo yao ya kazi wanayoyasimamia.