Ujumbe kutoka Shirika la Misaada la Marekani (USAID) wafanya ziara Sekretarieti ya Maadili.


Ujumbe kutoka Shirika la Misaada la Marekani (USAID) wafanya ziara Sekretarieti ya Maadili.
11
Oct
2017

Ujumbe kutoka Shirika la Misaada la Marekani (USAID) umefanya ziara fupi katika Ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Makao Makuu jijini Dar es Salaam na kufanya mazungumzo na uongozi wa taasisi hiyo.

Ujumbe huo ulioongozwa na Meneja Miradi wa Shirika hilo Bibi Florida Henjewele ulikuwa na lengo la kupitia “Mpango Kazi wa Mradi wa Kujenga Uelewa kwa Umma kuhusu shughuli zinazotekelezwa na Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma” unaofadhiliwa na Shirika hilo kabla ya kuanza utekelezaji wake hivi karibuni.

Moja ya shughuli zinazotekelezwa kupitia mradi huo ni kuandaa midahalo ya kitaifa itakayozungumzia namna ya kuunganisha mifumo ya usimamizi wa Maadili kupitia Maadhimisho ya Siku ya Maadili nchini.

Akizungumzia kuhusu shughuli hiyo Mkurugenzi wa Mipango na Tathmini wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambaye ni Msimamizi wa Mradi huo Bw. Omar Juma alisema kuwa shughuli hiyo itatekelezwa kwa pamoja na Taasisi nyingine za umma zinazosimamia Maadili na Utawala Bora nchini.

Aidha, midahalo hiyo inalengo la kuwakutanisha wadau mbalimbali wa masuala ya maadili na utawala bora nchini na kujadili namna nzuri ya kusimamia maadili na utawala bora ambapo itasaidia kukabiliana na vitendo vya rushwa hivyo kuchochea kasi ya maendeleo katika nchi yetu.

Kwa mujibu wa Bw. Omar maadhimisho ya mwaka huu yataratibiwa kwa kushirikiana na taasisi simamizi za masuala ya utawala bora nchini chini ya uwenyekiti wa Sekretarieti ya Maadili na kwamba kila taasisi itachangia kiasi fulani cha pesa ili kufanikisha shughuli hiyo.

Pia, sambamba na maadhimisho ya Siku ya Maadili, Bw. Omar alisema kuwa kutakuwa na uzinduzi wa klabu za maadili katika Shule za Msingi, Sekondari na vyuo ikiwa ni moja ya shughuli katika mradi huo yenye lengo la kuhamasisha maadili mashuleni.

Kwa mujibu wa mpango kazi wa mradi huo, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma inatarajia kufungua vilabu vya maadili katika baadhi ya shule za msingi na sekondari katika kanda nne ambazo ni eneo linalotekelezwa mradi huo. Kanda hizo ni Kanda ya Kusini (Mtwara), Kanda ya Kati (Dodoma), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya) na Kanda ya Mashariki (Pwani).

Pia, eneo lingine lililojadiliwa katika mazungumzo hayo ni mpango wa Sekretarieti ya Maadili wa kutaka kubadilisha mfumo wa namna ya kujaza Fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni kwa Viongozi wa Umma kutoka mfumo unaotumika sasa kwenda Mfumo wa kieletoniki yaani “Online Declaration System”.

Kuhusu mpango huo, Bw. Omari alisema kuwa wazo la kuwa na mfumo huo lilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah Kairuki (Mb) ambaye aliitaka Sekretarieti ya Maadili kufikiria mfumo mzuri utakaowarahisishia Viongozi wa Umma kujaza fomu za tamko na kuziwasilisha kwa Kamishna wa Maadili.

Kwa mujibu wa Bw. Omari, tayari Sekretarieti ya Maadili wameshaanza mazungumzo na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ambao wameonesha nia ya kuufadhili mpango huo ambapo alitumia fursa hiyo kuliomba Shirika la Misaada la Marekani (USAID) kutoa msaada wa rasilimali fedha na utaalamu ili kufanikisha mpango huo.

Naye Kiongozi wa Ujumbe huo Bibi Florida Henjewele aliiomba Sekretarieti ya Maadili kutekeleza mradi huo kwa umakini mkubwa kwa kuzingatia mpango kazi waliojiwekea. Aidha, Bibi Henjewele alisema kuwa Sekretarieti ya Maadili isisite kuomba ushauri au ufafanuzi kuhusu mradi huo wakati wowote watakapohitaji.

Mradi wa Kujenga Uelewa kwa Umma kuhusu shughuli zinazotekelezwa na Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma unafadhiliwa na USAID na unatekelezwa kwa mwaka wa tatu ambapo ulianza kutekelezwa tangu mwaka 2013.