Viongozi Wa Umma Kuhakikiwa Mali Zao.


 Viongozi Wa Umma Kuhakikiwa  Mali Zao.
13
Jun
2018

Sekretarieti ya Maadili ya viongozi wa umma inatarajia kufanya uhakiki wa rasilimali na madeni ya Viongozi nchi nzima ikiwa ni moja ya majukumu yanayotekelezwa na Sekretarieti hiyo.

Zaidi ya Viongozi 946 wanatarajiwa kufanyiwa uhakiki wa rasilimali na madeni yao kuanzia tarehe 18/06/2018. Viongozi hao ni wale wanaowajibika na Sheria ya Maadili ya namba 13 ya mwaka 1955 pamoja na marekebisho yake.

Hayo yalisemwa na Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Harold Nsekela alipozungumza na waandishi wa habari mapema wiki hii katika ukumbi wa mikutano wa ofisi hizo jijini Dar es Salaam.

Mhe Nsekela alifafanua kuwa lengo la uhakiki huo ni kuthibitisha uhalisia wa mali na madeni ya viongozi hao na kulinganisha na Tamko la Rasilimali na Madeni ya Kiongozi husika, thamani halisi ya mali hizo na uhalali wa mali hizo kwa kuangalia namna mali hizo zilivyopatikana.

Aidha Mhe.Nsekela katika hotuba yake amewataka viongozi wote ambao hawakuwasilisha nyaraka zao kufanya hivyo wakati wa zoezi la uhakiki.

Mhe. Nsekela aliongeza kwa kusema kuwa zoezi la uhakiki litafanyika nchini kote ambapo kila kiongozi anayetakiwa kuhakikiwa ataandikiwa barua kwanza ili aweze kujua rasilimali na madeni yatakayohakikiwa na kuandaa nyaraka mbalimbali za mali hizo ili waweze kuwaonyesha maafisa wa Sekretarieti wakati wa zoezi hilo.

Pamoja na hayo Mhe. Nsekela aliongeza kuwa lengo la barua hiyo pia ni kuepusha watu wenye nia ovu kutumia uwepo wa zoezi la uhakiki kutapeli viongozi kwa kuwatisha ili kujipatia manufaa mbalimbali kiuchumi.

Aidha Mhe. Nsekela alisisitiza kuwa Viongozi watakaohusika na zoezi la uhakiki wawatake maafisa wa Sekretarieti kuwaonyesha vitambulisho vyao,na kama Kiongozi hajaridhika na utambulisho huo anaweza anaweza kuwasiliana na Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili kupitia simu Na. 0222111810/11.

Hivyo basi Viongozi wanaombwa kutoa ushirikiano wa dhati wakati wa zoezi la uhakiki ili zoezi hilo liweze kuanikiwa kwa asilimia kubwa jambo ambalo litaiwezesha Sekretarieti ya Maadili kutekeleza majukumu yake ipasavyo.Kwa kufanya hivyo Viongozi watakua wamechangia kujenga uzalendo nchini kwani Maadili ni Nidhamu,Nidhamu inajenga Uwajibikaji,Utu na Haki kuelekea Uchumi wa Kati wa Viwanda.