Waziri Kairuki asisitiza Umuhimu wa Matumizi ya Teknolojia


Waziri Kairuki asisitiza Umuhimu wa Matumizi ya Teknolojia
26
Jul
2017

Mipango yote ya kuimarisha ufuatiliaji wa vitendo vya ukiukwaji wa maadili ya uongozi miongoni mwa viongozi wa umma ni nyeti na inahitaji kubadilika kulingana na mabadiliko ya tekonolojia duniani.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora Mhe. Angellah Kairuki (Mb), wakati akizindua Mfumo wa Kielektroniki wa Menejimenti ya taarifa za Kimaadili (EMIS) jijini Dar es salaam.

Aidha, Mhe. Kairuki alisema kuwa juhudi zinazofanywa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma za kuanzisha Mfumo wa kielektoniki wa kushughulikia masuala ya kimaadili zinapaswa kupongezwa kwani zitasaidia kujenga usikivu na uwajibikaji miongoni mwa viongozi wa Umma

Mhe. Kairuki aliitaka Sekretarieti kuongeza kasi katika usimamizizi wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma bila woga na kuongeza kuwa ni muhimu kwenda sambamba na kasi ya ukuaji wa teknolojia ya Habari na Mawasiliano jambo ambalo likipewa msukumo wa kutosha ni daraja muhimu la kujenga mahusiano kati ya Taasisi za Umma na Wananchi.

Pamoja na hayo Mhe. Kairuki aliongeza kuwa Mfumo huo wa kuchakata na kutunza taarifa mbalimbali za kimaadili utarahisisha upatikikanaji wa taarifa kwa wakati na ubora unaotakiwa pamoja na kupunguza gharama za ofisi. Pia, Mfumo huo utasaidia kupunguza hatari ya kupotea kwa nyaraka katika mchakato wa usafirishaji wa nyaraka hizo kutoka sehemu moja hadi nyingine na kupunguza muda wa kushughulikia na kutuma taarifa mbalimbali za masuala ya maadili na kuongeza kuwa mfumo huo ni moja ya utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kuhakikisha inatoa huduma bora kwa Wananchi na hivyo kurahisisha maendeleo ya nchi.

Awali, akimkaribisha mgeni rasmi Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji (Mst.) Harold Nsekela alisema kuwa lengo la Mfumo huo ni kurahisisha utendaji kazi wa watumishi kwa kutumia teknolojia ya kisasa zaidi kuliko ilivyo hivi sasa ambapo mfumo unaotumika ni Mfumo Mgumu yaani “Manual System.

Mhe. Kamishna aliongeza kuwa mfumo huo utawezesha kukusanya, kuchakata, kutunza taarifa na kumbukumbu mbalimbali kutoka kwa Viongozi wa Umma kuhusu mali na madeni waliyonayo wao binafsi na familia zao kwa kila mwaka. Pia, mfumo huo utasaidia kupata taarifa kuhusu malalamiko ya ukiukwaji wa maadili unaofanywa na viongozi wa umma dhidi ya wananchi wao. Mfumo wa Kielectroniki wa Menejimenti ya Taarifa za Kimaadili (EMIS) ni sehemu ya ufadhili uliotolewa kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kutoka Serikali ya Canada.